Shabaha
- Kueleza maana ya shina la neno
- Kutaja sifa za shina la neno
- Kutaja aina tatu za mashina
- Kuelezea kuhusu aina tatu za mashina.
Kufikia mwisho wa somo, mwanafunzi aweze:
Kudurusu
- Neno ni kitengo kidogo cha lugha. Huundwa kwa silabi ambazo zimefungamanishwa na kuleta maana.
- Mzizi wa neno ni sehemu ya neno ambayo inabeba maana halisi ya neno. Sehemu hiyo ya neno haibadiliki hata neno linapowasilishwa katika kauli tofauti.
- Aina mbili kuu za mizizi katika lugha ya Kiswahili ni:
- Mzizi tegemezi
- Mzizi huru.
- Aina mbili za mzizi tegemezi ni:
- Mzizi asilia
- Mzizi mnyumbuliko.
Maagizo
Kwa kutumia ubunifu na maneno yako mwenyewe, andika maelezo mafupi juu ya somo hili kwenye kitabu chako cha mazoezi unapoendelea kusoma na kisha uwasilishe maelezo yako kwa mwalimu wako wa lugha ya Kiswahili ili kuwezesha uhakiki na maoni yanayofaa.
Msamiati
Beba: Carry
Fungamanisha: Bind
Gawa: Divide
Halisi: Real
Kauli: Statement
Kiambishi: Affix
Maana: Meaning
Maoni: Comments/Feedback
Msingi: Foundation
Mzizi: Root of a word
Neno: Word
Rejelea: Refer
Sehemu: Part
Shina: Stem of a word
Shina ambatani: Compound word
Shina changamano: Root verb
Shina sahili: Root word
Sifa: Characteristics/Features
Ubunifu: Creativity
Uhakiki: Review
Wasilisha: Present
Wingi: Plural.
Shughuli 1: Maana ya shina
Shina ni neno lenye maana kamili, na ambalo haliwezi kugawanywa kwa misingi ya mzizi na viambishi. Neno lote ni mzizi. Shina linaweza kusimana pekee na kuleta maana.
Wingi wa shina ni mashina.
Shughuli 2: Sifa za shina
Zifuatazo ni baadhi ya sifa za shina:
- ni neno kamili
- linaweza kusimama pekee yake na kuleta maana
- linabeba maana halisi ya neno
- linaweza kutumika lilivyo kama mzizi wa kuundia neno jipya
- haliwezi kugawika zaidi bila kupoteza au kubadili maana ya neno.
Shughuli 3: Aina tatu za mashina
Aina tatu za mashina katika lugha ya Kiswahili ni:
- Shina sahili
- Shina changamano
- Shina ambatani.
Shughuli 4: Shina sahili
Shina hili hurejelewa pia kama mzizi huru. Hili ni shina lililoundwa kwa mofimu huru moja tu yenye maana kamili. Ni neno huru ambalo haliwezi kugawika zaidi bila kupoteza maana yake.
Mifano:
shangazi
jana
rafiki
chupa
babu
kesho
nyanya
simba
kitabu
baba
nyumba
kalamu
Shughuli 5: Shina changamano
Hili ni shina lililoundwa kwa kufungamanisha mzizi wa neno na kiambishi tamati katika kauli ya kutenda ‘-a’.
Mifano:
pig+a
andik-a
lip-a
osh-a
chez-a
imb-a
fagi-a
tazam-a
lim-a
shik-a
beb-a
wek-a
Shughuli 6: Shina ambatani
Hili ni shina lililoundwa kwa kuambatanisha mofimu huru mbili, ambazo pamoja huwa mzizi wa neno.
Mifano:
mbwamwitu
babamkwe
mwanasayansi
wazimamoto
garimoshi
mwananchi